Katibu Muthoni asema MPOX bado ni tishio nchini Kenya

Amehimiza Wakenya kuchukua tahadhari zinazohitajika huku mamlaka za afya zikiongeza ufuatiliaji na uhamasishaji wa umma.

Marion Bosire
1 Min Read
Mary Muthoni - Katibu katika Wizara ya Afya

Wakenya wamehimizwa kuwa waangalifu zaidi dhidi ya virusi vya MPOX, huku Wizara ya Afya ikionya kuwa ugonjwa huo bado ni tishio kubwa nchini.

Akizungumza Jumatatu, Katibu wa Idara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema MPOX bado inaendelea kuenea katika jamii, hasa maeneo ya mipakani na kwenye njia kuu za usafirishaji.

Aliwataka Wakenya kuchukua tahadhari zinazohitajika huku mamlaka za afya zikiongeza ufuatiliaji na uhamasishaji wa umma.

Kaunti saba zimetajwa kuwa katika hatari kubwa zaidi, zikiwemo Mombasa, Nairobi, Busia, Makueni, Kiambu, Kilifi na Nakuru, huku Mombasa ikirekodi idadi kubwa zaidi ya visa.

Hadi sasa, Kenya imethibitisha visa 1,298 vya MPOX katika kaunti 40 kati ya 47, huku watu 19 wakiripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Wizara imeitaka serikali kuimarisha ukaguzi katika vituo vya mipakani na kuendelea kutoa elimu kwa umma, ikionya kuwa Kenya bado haijatoka katika hatari hiyo.

Wakati huo huo, wizara imesema hakuna kisa cha Ebola kilichothibitishwa nchini, lakini imeweka mikakati ya kugundua na kudhibiti visa vyovyote vinavyoshukiwa.

Kuhusu mvua za El Niño zinazotarajiwa, Muthoni alisema wizara itafanya mkutano na wadau Jumatano kutathmini maandalizi. Kaunti 18 zimetajwa kuwa katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mvua hizo pamoja na magonjwa yatokanayo na maji.

Share This Article