EACC, SPSC ya China kushirikiana kuimarisha vita dhidi ya ufisadi

Martin Mwanje
2 Min Read
Mkurugenzi Mkuu wa SPSC Wang Xingning akiwa na uongozi wa EACC

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) itashirikiana na Tume Simamizi ya Jimbo la Shaanxi (SPSC) ya China katika kuimarisha vita dhidi ya jinamizi la ufisadi nchini. 

Hayo yaliafikiwa wakati uongozi wa EACC ulipokuwa mwenyeji wa ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Jamhuri ya Watu wa China ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa SPSC Wang Xingning.

Pande zote mbili zilijadiliana njia mwafaka za kuimarisha ushirikiano kati yao katika kuangamiza uovu huo wakati zikibadilishana uzoefu, mitazamo na namna ya kuendeleza uadilifu, uwajibikaji na uwazi katika utendaji kazi wao.

Mwenyekiti wa EACC Dkt. David Oginde alielezea shauku ya tume hiyo kujifunza tajiriba na mbinu zinazotumiwa na China katika kuzuia na kukabiliana na ufisadi, akielezea umuhimu wa kubadilishana maarifa na mbinu bora za kuimarisha jitihada za kupambana na ufisadi.

Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Abdi Mohamud aliangazia umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya EACC na SPSC na kuelezea utayari wa tume hiyo kushirikiana katika utafiti, mafunzo na ushirikishanaji wa maarifa ili kuboresha jitihada za kupambana na ufisadi.

Kwa upande wake, Wang alisema ufisadi unasalia changamoto ibuka na ngumu, huku wanaohusika katika uovu huo wakibadilika kama kinyonga kwendana na mazingira.

Alisisitiza umuhimu wa taasisi za kupambana na ufisadi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuangazia changamoto ibuka.

Mkutano huo  ulisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi na kuhamasisha uadilifu, uwazi na uwajibikaji.

 

Share This Article