Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imewasilisha kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ikiishutumu kwa ukatili wa miongo mitatu mashariki mwa taifa hilo.
Serikali ya DRC iliwasilisha kesi hiyo siku ya Ijumaa, ikiishtumu Kigali kwamba iliwajibika kwa visa vya mauaji, watu kuhama makwao na visa vingine vya ukatili, mashariki mwa taifa hilo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini.
Kulingana na DRC, ukatili huo ulichangiwa na kuwepo wa makundi mengi yenye silaha ikiwa ni pamoja na kundi la M23, ambalo limeteka maeneo makubwa mashariki mwa DRC. Kundi hilo linadaiwa kupata ungwaji mkono na Rwanda, licha kwamba Kigali imekanusha madai hayo.
Kupitia kwa taarifa, Mahakama ya ICJ imesema DRC inaishutumu Rwanda kwa makosa yaliyofanywa kati ya mwaka 1996 hadi sasa, na kwamba wanaolengwa ni jamii ya wahutu kutokana na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Aidha, kwenye kesi hiyo, DRC imesema makabila mengine pia yalilengwa yakiwa ni pamoja na Nyindu, Bembe, Lega, Nande, Hunde na Bashi.