Serikali yahimizwa kukabiliana na magenge ya wahuni

Tom Mathinji
2 Min Read
Kongamano la maaskofu wa kanisa katoliki.

Kongamano la Maaskofu wa Kanisa Katoliki hapa nchini (KCCB) limeelezea wasiwasi  wake kuhusu kuibuka tena kwa makundi ya wahuni, likionya kuwa utumizi wa ghasia kuvuruga mikutano unahujumu haki ya kidemokrasia.

Maaskofu hao walisema vurugu zilizoshuhudiwa katika mkutano ulioandaliwa katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi, pamoja na visa sawa na hivyo kwenye maeneo ya ibada, zinaashiria ongezeko la hali ya kutojali sheria.

Kwenye taarifa, Maaskofu hao walitoa wito kwa serikali kushughulikia wasiwasi unaoibuliwa na wananchi dhidi ya wahuni kupewa silaha kuwatishia wale wanaohudhuria mikusanyiko halali ya umma.

“Tuna wasiwasi kwamba wahuni wanaungwa mkono kirasmi. Serikali inaweza kuondoa hofu hii kutoka kwa mawazo ya Wakenya? Je, kuna nia ya kisiasa kushughulikia tatizo la uhuni?”, walishangaa Maaskofu hao.

Viongozi hao wa dini walitoa wito kwa wanasiasa kuheshimu sehemu za ibada, wakisema ni maeneo yaliyolindwa na hayapaswi kugeuzwa kuwa uwanja wa malumbano.

Taarifa hiyo inajiri huku polisi wakiendelea kuchunguza kisa ambapo wahuni walivuruga mkutano katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi siku chache zilizopita.

Aidha, Maaskofu hao wamemtaka Inspekta Mkuu wa Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vurugu hizo, kuwatambua wahusika na kuwafungulia mashtaka.

Maaskofu hao walikuwa wakizungumza kabla ya kikao cha 21 cha Muungano wa Wajumbe wa Makongamano ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) kilichopangwa kuandaliwa jijini Nairobi mwezi ujao.

Share This Article