Lukwago akosa kufika mahakamani kisa matibabu

Mamlaka ya Magereza ya Uganda iliieleza mahakama kwamba Lukwago anaendelea kupatiwa matibabu maalumu.

Marion Bosire
2 Min Read
Erias Lukwago, Meya wa zamani wa Kampala, Uganda

Meya wa awali wa Jiji la Kampala, Erias Lukwago, hakufikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkuu ya Makindye leo, Jumanne, tarehe 30 Juni 2026, kama ilivyotarajiwa, kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi inayomkabili ya kutofichua njama za uhaini.

Mamlaka ya Magereza ya Uganda iliieleza mahakama kwamba Lukwago anaendelea kupatiwa matibabu maalumu.

Baada ya mkutano uliofanyika katika ofisi ya hakimu, wakili mkuu wa utetezi wa Lukwago, Medard Lubega Sseggona, aliambia waandishi wa habari kwamba Jeshi la Magereza la Uganda lilikuwa limeiandikia mahakama kueleza sababu zilizomfanya mwanasiasa huyo wa upinzani ashindwe kufikishwa mahakamani.

“Lukwago hakufikishwa na magereza hapa leo. Sababu ni kwamba anaendelea kupatiwa matibabu maalumu. Hivyo, Jeshi la Magereza la Uganda limeiandikia mahakama na kuifahamisha kuwa aliyekuwa Meya wa Jiji la Kampala hayupo hapa kutokana na uchunguzi wa kitabibu unaoendelea,” alisema Sseggona.

Aliongeza kuwa hali ya afya ya Lukwago imezorota na kwamba madaktari wameona kuwa hana uwezo wa kuhudhuria mahakamani kwa sasa.

Lukwago ambaye ni kiongozi wa upinzani na Wakili alikamatwa kutoka nyumbani kwake huko Wakaliga jijini Kampala Juni 15, 2026.

Alizuiliwa bila kuruhusiwa kuwasiliana na yeyote kwa siku kadhaa na baadaye alifikishwa katika mahakama ya Hakimu, ambapo alishtakiwa rasmi kwa kosa kutoripoti kosa la uhaini na kuwekwa rumande.

Kisa hiki kiliibua hisia kali nchini Uganda, ikikumbukwa kwamba Lukwago ni mwanasiasa mashuhuri wa upinzani na wakili wa kiongozi anayezuiliwa kwa uhaini, Kizza Besigye.

Share This Article