Mkuu wa zamani wa wafanyakazi katika Ikulu ya Nairobi Nzioka Waita ametangaza kuwa atajaribu bahati tena kwa kugombea wadhifa wa Ugavana wa kaunti ya Machakos kwa tiketi ya chama tawala cha UDA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Waita amesema wakazi wa kaunti ya Machakos wamekosa maendeleo kutokana na kile alichodai ni uhusiano duni kati ya Gavana Wavinya Ndeti na Rais William Ruto.
Amewataka wakazi wa kaunti hiyo kumchagua ili kuharakisha maendeleo.
Aidha, Waita amemkosoa Gavana Ndeti kwa kumhusisha na madai ya ubadhirifu wa fedha.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Waita aligombea Ugavana wa kaunti ya Machakos kwa tiketi ya Chama cha Uzalendo (CCU) na kubwagwa na Gavana Ndeti aliyegombea kiti hicho kwa chama cha Wiper.
Mbunge wa Mavoko Patrick Makau pia ametangaza kuwa atagombea Ugavana wa Machakos kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Taarifa ya Jonathan Musau