Katibu Mugambi atetea ujenzi wa uwanja wa ndege msituni Imenti

Amesisitiza kwamba dhamira ya serikali ni kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Marion Bosire
3 Min Read
Gitonga Mugambi, Katibu wa Idara ya Misitu

Serikali ya Kitaifa imetetea uamuzi wake wa kujenga uwanja wa ndege ndani ya Msitu wa Imenti ulioko Kaunti ya Meru, huku ikikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa wahifadhi mazingira na baadhi ya wananchi.

Mradi huo unaopendekezwa, ambao pia unahusisha ujenzi wa Ikulu ndogo, umeibua mjadala mkubwa.

Wanaharakati wa mazingira wameeleza wasiwasi kwamba maendeleo hayo yanaweza kuathiri mfumo ikolojia wa msitu na kuhatarisha mojawapo ya maeneo muhimu ya vyanzo vya maji nchini.

Hata hivyo, Katibu wa Idara ya Misitu katika Wizara ya Mazingira, Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi Gitonga Mugambi, amekanusha madai kwamba mradi huo utasababisha uharibifu wa mazingira.

Amesisitiza kwamba dhamira ya serikali ni kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, uwanja wa ndege unaopendekezwa utatumika kama kituo cha shughuli za uangalizi na ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali ndani ya mfumo ikolojia wa Msitu wa Mlima Kenya.

Alisema kituo hicho kitawezesha taasisi za serikali kuitikia haraka matukio kama ukataji haramu wa miti, uchomaji makaa, uvamizi wa misitu, moto na vitisho vingine vya kiusalama vinavyoathiri msitu.

Mugambi aliongeza kuwa uwanja huo utaimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa serikali wa kukabiliana na dharura kwa kuwezesha kupelekwa haraka kwa maafisa na vifaa wakati wowote kunapotokea tukio la dharura katika maeneo makubwa ya msitu.

Aidha, alifichua kuwa serikali inapanga kutumia ndege katika mipango ya baadaye ya urejeshaji wa misitu, hasa katika maeneo ambayo ni magumu kufikika kwa barabara au kwa miguu.

Kupitia usambazaji wa mbegu kutoka angani, mbegu za miti ya asili zitapandwa katika sehemu za mbali za msitu huo ili kuharakisha juhudi za urejeshaji na kuongeza uoto wa misitu.

Katibu huyo alisisitiza kuwa maendeleo yote yaliyopangwa yatafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni za mazingira, na kwamba yanalenga kuimarisha juhudi za uhifadhi badala ya kuzidhoofisha.

Licha ya maelezo hayo kutoka serikalini, pendekezo hilo linaendelea kuzua maoni kinzani.

Wanaharakati wa mazingira na makundi ya uhifadhi wameitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na ushirikishaji mpana wa umma pamoja na uwazi zaidi.

Walisisitiza kuwa maendeleo yoyote ndani ya maeneo ya misitu iliyohifadhiwa yanapaswa kupitia tathmini ya kina ya athari kwa mazingira kabla ya kutekelezwa.

Kwa upande mwingine, wanaounga mkono mradi huo wanaamini kuwa uwanja wa ndege uliopendekezwa utaimarisha usalama, kuboresha usimamizi wa misitu na kuimarisha shughuli za uhifadhi ndani ya mfumo wa ikolojia wa Mlima Kenya.

Wakati mjadala kuhusu mradi huo ukiendelea, serikali inasisitiza kuwa miundombinu hiyo inalenga kulinda rasilimali za asili za nchi huku ikiboresha ufanisi wa shughuli za uhifadhi wa misitu.

Share This Article