Washukiwa wawili wa uhalifu wakamatwa Narok

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wawili wa uhalifu wakamatwa Narok.

Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wawili wa  uhalifu katika kituo cha kibiashara cha Mau-Narok, ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi katika eneo hilo.

Wawili hao walikamatwa baada maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Mau-Narok, kutekeleza operesheni iliyolenga kukabiliana na visa vya uhalifu vilivyotajwa kuongezeka katika eneo hilo.

Kupitia ukurasa wa X, Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema washukiwa hao walipatikana na silaha, ishara kwamba walilenga kutekeleza shughuli za uhalifu.

Polisi wamewahusisha washukiwa hao na genge la uhalifu la “Men in Black”, ambalo limedaiwa kutekeleza misururu ya wizi na ujambazi na kuwaathiri wafanyabiashara na wakazi wa Mau-Narok.

Wakati wa operesheni hiyo, washukiwa wawili zaidi walikamatwa wakiwa na mali ya wizi, na kuashiria mtandao mkubwa unaohusishwa na kuhifadhi na kusambaza mali ya wizi.

Washukiwa hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakani.

Share This Article