Wakazi wa Busia wataka Busaa ihalalishwe

Tom Mathinji
2 Min Read
Wakazi wa Busia wataka Busaa ihalalishwe.

Wakazi, wafanyabiashara na wadau wa kitamaduni wamewasilisha ombi katika Bunge la Kaunti ya Busia wakitaka kuhalalishwa, kudhibitiwa na kulindwa kwa ugemaji wa busaa, wakitaja kinywaji hicho kuwa na mizizi ya kitamaduni na thamani yake kiuchumi.

Mwanahabari wa zamani Kennedy Epalat, aliyewasilisha ombi hilo kwa afisa anayesimamia shughuli za bunge Oroni Patrick, alisema yuko tayari kulitetea huku akiwataka wawakilishi wadi kuishughulikia kwa haraka.

Alidokeza kuwa wakenya wengi huvuka mpaka kwenda nchi jirani ya Uganda kubugia kinywaji hicho ambacho nchini humo wananchi wamepewa muda maalum wa kuibugia.

Epalat alitaja busaa kuwa kinywaji kilichoandaliwa kwa njia ya kitamaduni kutoka kwa bidhaa za mahindi na mtama na ambacho hupamba uraibu wa wakazi Magharibi mwa Kenya.

Busaa, kulingana na mwanahabari huyo hutekeleza jukumu kubwa katika hafla za kitamaduni katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na sherehe za harusi, vijana kupelekwa jandoni, usuluhishaji mizozo na mikusanyiko mingine ya kijamii.

Bunge la Kaunti ya Busia, linatarajiwa kuchunguza ombi hilo kuambatana na kanuni za bunge na kutoa mapendekezo ya kisheria au kisera.

Ikiwa bunge hilo litahalalisha busaa, kaunti hiyo itaigwa na kaunti zingine kwa kutoa mikakati mwakafaka ya kuhalalisha baadhi ya vinywaji vya kitamaduni, kwa lengo la kuhifadhi utamaduni kwa kuzingatia mbinu za kisasa za udhibiti.

Share This Article