Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa kilichoshangaza wengi cha wizi wa kimabavu katika mkahawa fulani eneo la Westlands, Nairobi.
Washukiwa wanne wasiojulikana waliokuwa wakitumia pikipiki mbili walivamia mgahawa huo, wakawaibia wateja vitu vyao vya thamani, wakafyatua risasi mbili hewani na kutorokea upande wa Parklands.
Ganda moja la risasi ya milimita 9 lilipatikana katika eneo la tukio.
Wapelelezi hadi sasa wamehoji baadhi ya waathiriwa, huku waathiriwa na mashahidi wengine wakitarajiwa kutoa taarifa zao uchunguzi unapoendelea.
Maafisa wa Kitengo cha Picha na Uchambuzi wa Sauti wanaendelea kurejesha na kuchambua picha za kamera za usalama kutoka eneo hilo.
Wakati huo huo, wachunguzi wa eneo la tukio wamewasilisha ushahidi muhimu uliokusanywa huko kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi.
Uchunguzi unaoongozwa na taarifa za kijasusi na ushahidi wa kisayansi unaendelea, huku juhudi zikielekezwa katika kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani washukiwa husika.
Idara ya Upelelezi wa Jinai inahimiza yeyote aliye na taarifa muhimu awasiliane na maafisa wake katika kituo cha Gigiri, kituo cha polisi kilicho karibu naye, au kupitia #FichuaKwaDCI kwa kupiga simu ya bure nambari 0800 722 203 au kutuma ujumbe wa WhatsApp kwa 0709 570 000.
Huku hayo yakijiri, DCI inahakikishia umma kuhusu kujitolea kikamilifu kulinda usalama wa watu wote ndani ya Jamhuri na kuhakikisha wanaohusika na vitendo vya uhalifu wanawajibishwa na kufikishwa mbele ya sheria.