Wingu la huzuni lilitanda wakati wa ibada ya wafu ya wanafunzi 16 waliofariki kwenye mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru ikiendelea.
Mkewe Rais, Rachel Ruto na Waziri wa Elimu Julius Ogamba, ni miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo katika uwanja wa Gilgil.
Wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa wakati wa mkasa huo uliotokea Mei 28.
Majeruhi wote wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku wanafunzi 9 wanaoshukiwa kuwasha moto na kutekeza bweni la shule hiyo wakizuiliwa kupisha uchunguzi wa kina.
Katika uwanja wa Gilgil, wazazi na jamaa wa marehemu walielemewa na uchungu wa kuwapoteza wanao waliowategemea katika siku za baadaye maishani.

Uhai wa wanao ukikatizwa ghafla na kisa ambacho serikali imekitaja kuwa uwashaji wa moto kimakusudi unaoshukiwa kufanywa na yamkini wanafunzi 9 watundu wa shule ya Utumishi Girls Academy usiku wa manane wakati wenzao walizamia usingizini.
Maafisa wa upelelezi bado wanakichunguza kisa hicho kwa mapana na marefu.
Tangu tukio la Utumishi Girls Academy, shule 204 zilifungwa nchini kutokana na visa vya utovu wa nidhamu na vurugu za wanafunzi huku shule 59 kati ya shule hizo zikirejelea masomo.
Serikali imeapa kukabiliana vikali na wanafunzi watundu wanaotatiza kalenda ya masomo ya mamia ya shule nchini.