Mkuu wa chuo cha ubaharia ahimiza matumizi ya AI kubadilisha sekta hiyo

Dkt. Katana anasema suluhisho zinazoendeshwa na AI zinabadilisha sekta ya ubaharia kwa kuongeza ufanisi wa shughuli, kuimarisha usalama baharini na kuwawezesha wataalamu wa baadaye wa masuala ya ubaharia kupata ujuzi unaokidhi mahitaji yanayobadilika ya sekta hiyo duniani.

radiotaifa
2 Min Read
Dkt. Eric Katana - Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Ubaharia cha Bandari (BMA)

Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Ubaharia cha Bandari (BMA), Dkt. Eric Katana ametoa wito wa matumizi ya akili unde, AI katika elimu na mafunzo ya masuala ya ubaharia, akisisitiza umuhimu wake unaozidi kuongezeka katika kuunda mustakabali wa sekta ya ubaharia na uchumi samawati.

Akizungumza wakati wa mjadala wa jopo kuhusu teknolojia za uchumi samawati na AI katika Kongamano la Masuala ya Baharini almaarufu almaarufu Our Ocean Conference 2026, Dkt. Katana alisema kuwa suluhisho zinazoendeshwa na AI zinabadilisha sekta ya ubaharia kwa kuongeza ufanisi wa shughuli, kuimarisha usalama baharini na kuwawezesha wataalamu wa baadaye wa masuala ya ubaharia kupata ujuzi unaokidhi mahitaji yanayobadilika ya sekta hiyo duniani.

“Akili Unde si dhana ya siku zijazo tena; ni nyenzo inayotumika sasa na inayobadilisha namna tunavyofundisha, kuendesha shughuli na kuibua ubunifu katika sekta ya ubaharia. Taasisi zinapaswa kukumbatia teknolojia hizi ili ziendelee kuwa na umuhimu na ushindani,” alishauri Dkt. Katana.

Aidha, alisisitiza dhamira ya BMA kuendelea kuingiza teknolojia za kisasa katika programu zake za mafunzo, hatua ambayo inakiweka chuo hicho kama kituo cha umahiri katika elimu ya masuala ya ubaharia na uchumi samawati katika ukanda huu.

Kauli zake zilijiri wakati kongamano hilo lilipoanza rasmi katika hoteli moja mjini Mombasa, likiwaleta pamoja viongozi wa kimataifa, watunga sera, watafiti na wataalamu wa sekta mbalimbali kujadili suluhisho bunifu za uhifadhi wa bahari na matumizi endelevu ya rasilimali za baharini.

Kongamano hilo linaashiria hatua muhimu katika juhudi za kimataifa za kuimarisha usimamizi endelevu wa bahari na kukuza sekta ya uchumi samawati.

Washiriki wanazamia katika mijadala ya ngazi ya juu kuhusu teknolojia zinazoibuka, utunzaji wa mazingira na mikakati ya kulinda mifumo ikolojia ya baharini huku wakichochea ukuaji wa uchumi.

Kongamano hilo linatarajiwa kuzaa ahadi za utekelezaji na ushirikiano wa kimkakati ambao utaharakisha utekelezaji wa mbinu endelevu za usimamizi wa bahari na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda bahari za dunia kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Share This Article