Asasi za usalama zahimizwa kudumisha usalama wakati wa maandamano ya Gen Z

Tom Mathinji
1 Min Read
Polisi watakiwa kukabiliana na magenge ya wahalifu wakati wa maandamano ya Gen-Z ya Juni 25,2026.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu limetoa wito kwa asasi za usalama kukabiliana vilivyo na magenge ya wahuni wakati wa maandamano ya Gen Z yatakayoandaliwa Juni 25, 2026.

Maandamano hayo yanaandaliwa kuwakumbuka waliofariki kwenye maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Wakizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza hilo, wazee hao walimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuhakikisha amani inadumishwa na maandamano hayo hayavurugwi na wahuni.

Kupitia kwa taarifa iliyosomwa na Katibu Mkuu wa baraza hilo James Nene, wazee hao walisema udumishaji wa amani ni jukumu la pamoja, wakidokeza kuwa wazee wanajukumu la kutoa mwongozo kwa jamii, kutambua changamoto ibuka na kutoa onyo dhidi ya hatua zinazohujumu mshikamano wa kitaifa.

Aidha, baraza hilo lilidokeza kuwa Kenya imefurahia hali ya utulivu kwa muda mrefu, isipokuwa tu ghasia zilizochochewa kisiasa miaka ya 1992, 1997 na 2007.

Wakati huo huo, baraza hilo lilielezea wasiwasi kuhusiana na taharuki ya kisiasa na vurugu za kupangwa huku maandamano ya Gen Z yanapokaribia.

Waliwataka wanasiasa kutafakari kabla ya kuchukua hatua zozote zinazoweza kuvuruga uthabiti wa taifa.

Share This Article