Mradi muhimu wa kuboresha bandari ya Mombasa wa gharama ya shilingi bilioni 8.3, umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Mamlaka ya Bandari ya Kenya, KPA imeelezea imani kuwa mradi huo utabadilisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo na kupunguza msongamano katika bandari hiyo yenye shughuli nyingi zaidi nchini.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka ujao wa 2027 na ni sehemu ya mpango mpana wa KPA wa kuboresha miundombinu ya bandari na kuimarisha muunganiko wa njia muhimu za usafirishaji wa mizigo, kama Lango la 18, Lango la 20 na Barabara ya Kipevu.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, William Ruto, alisema mradi huo ni zaidi ya ujenzi wa barabara, akieleza kuwa ni makutano maalumu ya usafiri yaliyobuniwa kuondoa msongamano uliobainishwa katika utafiti uliofanywa na TradeMark Africa mwaka 2018.
Alisema zabuni ya mradi huo ilitolewa kupitia ushindani wa kimataifa na kutuzwa kwa ubia wa kampuni za Stecol Corporation na Miliki Development Company baada ya kuwasilisha zabuni ya chini yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.3, akiongeza kuwa mradi huo unatoa thamani halisi ya fedha zilizowekezwa.
Kazi zinazotekelezwa zinahusisha ujenzi wa barabara ya njia mbili yenye urefu wa kilomita 1.8, ikijumuisha daraja refu la juu lenye urefu wa mita 704, duru mbili za barabara, njia za kuingia na kutoka pamoja na njia za kuunganisha ili kurahisisha mtiririko wa malori ya mizigo.
Mshauri wa mradi, Mhandisi Stephen Wasike, alisema daraja hilo lilijengwa kwa kimo maalumu ili kupita salama juu ya mabomba ya mafuta na miundombinu iliyopo bandarini bila kuathiri shughuli za kila siku.
Mradi huo pia unahusisha uhamishaji wa miundombinu ya umeme, maji, nyaya za mawasiliano za fiber optic na mifumo ya usalama, pamoja na ujenzi wa mfumo wa kisasa wa kupitisha maji ya mvua ili kulinda bandari dhidi ya mafuriko na kuhakikisha shughuli zake zinaendelea kwa ufanisi kwa muda mrefu.