Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Masika Wetang’ula, amejaribu kutuliza wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa walimu kuhusu changamoto za kupata huduma za afya chini ya mpango wa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA.
Kiongozi huyo ameahidi hatua za haraka kushughulikia matatizo hayo.
Katika taarifa aliyotoa baada ya kuwa mwenyeji wa walimu wa Kaunti ya Bungoma nyumbani kwake, Wetang’ula alikiri kuwa changamoto zinazokumba walimu ni za kweli na zinahitaji kushughulikiwa kwa dharura.
Alifichua kuwa anatarajia kukutana na Waziri wa Afya, Adan Duale, wiki ijayo ili kujadili suluhisho za vitendo zitakazoboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa walimu chini ya mfumo huo mpya.
Spika huyo alibainisha kuwa walimu pia walieleza wasiwasi kuhusu utekelezaji wa mageuzi ya elimu, hasa wakitaka uhuru kamili kwa walimu wa Shule za Sekondari za Msingi au Junior Secondary School, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa mtaala.
Aidha, masuala ya usawa katika kupandishwa vyeo na ajira kwa walimu yaliibuliwa wakati wa mkutano huo, ambapo Wetang’ula aliahidi kushirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa masuala hayo yanashughulikiwa kwa uwazi na haki.
Wakati huo huo, alihimiza walimu kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Rais William Ruto, akisisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa walimu huku nchi ikiendelea kusonga mbele katika kufanikisha malengo yake ya maendeleo.