Daktari akamatwa kwa kukaribia chumba cha Besigye

Maafisa wa polisi hata hivyo walimwachilia kwa dhamana na kumwelekeza arejee kituoni Agosti 10, 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Ripoti za hivi punde kutoka Uganda zinaashiria kwamba Daktari mmoja amekamatwa kwa kuzurura zurura karibu na chumba alicholazwa mwanasiasa wa upinzani nchini humo Dkt. Kizza Besigye.

Daktari huyo aliyetambuliwa kama Moses Mukose alikamatwa katika hospitali ya kuu ya Mulago, walinzi wakimlaumu kwa kujaribu kuingia kwenye chumba cha mgonjwa huyo.

Maafisa wa polisi hata hivyo walimwachilia kwa dhamana na kumwelekeza arejee kituoni Agosti 10, 2026.

Besigye amelazwa hospitalini katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kuzirai mahakamani Jumatano Julai 29, 2026, ambapo kesi inayomkabili ya uhaini ilikuwa ikiendelea.

Siku hiyo Besigye ambaye afya yake ilionekana kudhoofika, alipaaza sauti na kufoka kwa dakika kadhaa kabla ya kuanguka chini, hali iliyowalazimu waliokuwemo mahakamani kuchukua hatua za haraka kumsaidia.

Mvutano mfupi ulizuka kati ya mawakili wa Besigye na askari wa magereza wakati wa juhudi za kumtoa kwenye kizimba na kumpatia huduma ya kwanza.

Tukio la kuanguka kwa Besigye liliibua wasiwasi miongoni mwa mawakili wa pande zote na watu waliokuwepo mahakamani siku hiyo huku kutotolewa kwa taarifa kuhusu hali yake kukizidisha hali.

Kanali Mstaafu Dkt. Kizza Besigye amekuwa kizuizini kwa mashtaka ya uhaini, huku kesi yake ikiendelea kusikilizwa mahakamani.

Share This Article