Bintiye Museveni kutawazwa kama askofu

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Agosti 23, 2026, katika kanisa la Covenant Hill lililoko eneo la Maya, nje tu ya mji wa Kampala.

Marion Bosire
1 Min Read

Binti ya Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na mkewe Janet Museveni, Patience Rwabwogo anakaribia kutawazwa kama askofu wa kanisa la Covenant Nations Churches in Uganda and beyond.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Agosti 23, 2026, katika kanisa la Covenant Hill lililoko eneo la Maya, nje tu ya mji wa Kampala.

Haya ni kwa mujibu wa bango la kutangaza hafla hiyo pamoja na mpangilio wa matukio wa siku hiyo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na binti huyo wa Rais.

Kwenye tangazo hilo, wageni wa heshima wa hafla hiyo wanajumuisha Rais Museveni na Mama Janet, hiyo ikitarajiwa kuwa siku ya kwanza ya mkewe Rais kuonekana hadharani tangu alipougua.

Tukio hilo vile vile litatumiwa kusherehekea miaka 20 ya uwepo wa kanisa la Covenant Nations ambalo Patience alianzisha na anaongoza.

Mhubiri Dkt. LaDonna Osborn ataendesha sherehe ya siku hiyo ya kumtawaza Pastor Patience huku Mhubiri Enoch Adejare Adeboye na mkewe na Pastor Folu Adeboye, wakiorodheshwa kama wageni mashuhuri.

Patience Museveni Rwabwogo, ndiye binti wa pili wa Rais Museveni aliyezaliwa mwaka 1978. Ameolewa na Odrek Rwabwogo.

Kando na kuwa mhubiri ameandika kitabu kiitwacho ‘Jesus’ Africa’.

Share This Article