Waziri wa masuala ya jinsia, utamaduni na huduma za watoto, Hannah Wendot Cheptumo amempongeza Rais william Ruto kwa kuleta sare mpya za polisi wajawaziti.
Katika taarifa Wendot alisema Rais ameendelea kudhihirisha kujitolea kwake kuendeleza utawala unaotambua jinsia na kutoa mazingira mwafaka kwa maafisa wa kike kuendelea kutoa huduma kwa umma.
“Kuletwa kwa sare makhsusi za polisi wajawazito wanaohudumu chini ya wizara ya masuala ya ndani na utawala wa kitaifa ni dhihirisho la kujitolea huko,” alisema Waziri huyo.
Cheptumo aliendelea kusema kwamba hatua hiyo inaonyesha uelewa kwamba usawa wa kijinsia hutiwa nguvu na hatua za kivitendo za kitaasisi zinazotambua hadhi, mahitaji na mchango wa wanawake katika maeneo ya kazi.
Kulingana naye, wanawake hutekeleza jukumu muhimu katika usalama na uhusika wao ni muhimu katika kujenga taasisi za usalama zenye kusikiliza, uwakilishi na zenye ufanisi.
Sare hizo pia alisema zinaendana na ajenda ya wanawake, amani na usalama hasa kanuni ya uhusika wa maana wa wanawake katika sekta ya usalama.
“Kuunga mkono wanawake kuhudumu na kujiendeleza ndani ya taasisi za usalama hukuza sio tu usawa wa kijinsia bali pia taasisi zenyewe,” alimalizia waziri huyo.
Taarifa yake inajiri saa chache baada ya Rais William Ruto kuzindua sare mpya za maafisa wa polisi ambazo kwa mara ya kwanza zinajumuisha za maafisa wajawazito.