Mbunge Kaluma atakiwa kufika mbele ya NCIC

Martin Mwanje
1 Min Read
Peter Kaluma - Mbunge wa Homa Bay Mjini

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC imemtaka mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma kufika mbele yake kuhusiana na matamshi anayodaiwa kutoa mwishoni mwa wiki iliyopita akitishia upande wa upinzani.

Kaluma alinukuliwa akisema yeyote anayepinga kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto katika eneo la Homa Bay anapaswa kukabiliwa vikali kwani eneo hilo ni ngome ya ODM.

Chama hicho kimetangaza kuwa kitaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Kwenye taarifa, NCIC imemtaka Kaluma kufika mbele yake kesho Jumatano kuelezea alichomaanisha kwenye matamshi yake ambayo pia yalitoa wito wa upekuzi wa hoteli za eneo hilo.

Lengo la upekuzi huo lilikuwa kuwafurusha wapinzani wa serikali saa chache kabla ya kuandaliwa kwa mkutano wa vuguvugu la Linda Mwananchi katika eneo hilo.

Juzi Jumapili, vurugu zilishuhudiwa katika kaunti ya Homa Bay wakati wa mkutano wa Linda Mwananchi ambao ulisababisha kujeruhiwa kwa wanahabari 8.

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS inasema watu 37 wamekamatwa kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo.

 

 

Share This Article