Jaji Mkuu Martha Koome amehimiza Mahakama ya Rufani kuharakisha utoaji wa haki na kupunguza mrundiko wa kesi zilizodumu muda mrefu huku Jaji Gatembu Kairu akichukua rasmi uongozi kama Rais mpya wa Mahakama ya Rufani.
Akizungumza katika hafla ya kumwapisha Jaji Kairu jijini Nairobi Jumatano, Koome alisema Mahakama ya Rufani ni nguzo muhimu ya mfumo wa haki nchini Kenya.
Koome alibainisha kuwa ndiyo mahakama ya mwisho katika kesi nyingi na ina jukumu muhimu la kuhakikisha tafsiri ya sheria inakuwa thabiti na yenye uwiano.
Alisema mahakama hiyo imepiga hatua kubwa katika miaka mitano iliyopita kwa kuongeza vituo vyake vya kudumu kutoka vinne hadi vinane na kuongeza idadi ya majaji kutoka 13 mwaka 2021 hadi 41 kufuatia uteuzi wa hivi karibuni.
Hata hivyo, Koome alisisitiza kuwa maelfu ya rufaa ambazo bado hazijasikilizwa zinaendelea kuwanyima Wakenya wengi haki kwa wakati.
Jaji Mkuu aliitaka Mahakama ya Rufani kuweka lengo la kusikiliza na kuamua kesi za rufaa ndani ya mwaka mmoja kutoka muda wa kuwasilishwa, kuongeza kiwango cha utatuzi wa kesi na kukumbatia teknolojia.
Alimalizia kwa kumpongeza Rais anayeondoka wa mahakama hiyo Jaji Daniel Musinga.
Jaji Gatembu Kairu aliahidi kuongoza mahakama hiyo kwa uwazi, ushirikishaji na utiifu kwa Katiba, akitaja kupunguza mrundiko wa kesi na kuharakisha usikilizaji wa rufaa kuwa vipaumbele vyake vikuu.
Pia aliahidi kuimarisha usimamizi wa mashauri, utafiti wa kimahakama na ushirikiano wa taasisi huku akihimiza utoaji wa maamuzi yenye msimamo unaofanana.