Maafisa wa usalama wamewakamata washukiwa saba wanaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya nyama katika eneo la Gatitu Muruguru, kaunti ya Nyeri.
Washukiwa hao walikamatwa baada ya maafisa wa usalama wakishirikiana na wale wa ukaguzi wa nyama, kutekeleza operesheni iliyosababisha kugunduliwa kwa sakata hiyo ya biashara haramu ya nyama iliyokuwa ikitekelezwa katika eneo hilo.
Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Kamishna wa Kaunti ya Nyeri Josephat Biwott, alisema washukiwa hao walipataikana wakichinja mifugo na kusambaza nyama ya mifugo hao bila kibali halali cha kuendeleza biashara hiyo.
Kulingana na kamishna huyo wa kaunti, maafisa hao walipata zaidi ya kilo 400 ya nyama ambayo haijakaguliwa, inayoaminika ilikusudiwa kusambazwa kwa wateja katika kaunti hiyo na maeneo yaliyo karibu.
Aidha, uchunguzi zaidi umebainisha kuwa biashara hiyo haramu huenda inahusishwa na visa vya wizi wa mifugo vinavyoongezeka katika sehemu za kaunti ya Nyeri.
Alionya kuwa serikali imeimarisha msako unaolenga wanaotekeleza biashara haramu ya nyama, visa vya wizi wa mifugo na wafanyabiashara wanaokiuka sheria.
Biwott alisisitiza kuwa utumizi wa nyama ambayo haijakaguliwa, ni hatari kwa afya ya binadamu.
Wakati huo huo aliagiza wasafirishaji wote wa mifugo na wafanyabiashara kuhakikisha wana vibali kabla ya kusafirisha mifugo kutoka kaunti hiyo.