Rais Samia azindua hospitali ya Julius Nyerere nchini Angola

Rais Samia ambaye yuko kwenye ziara rasmi nchini Angola, alizindua hospitali hiyo akiwa ameandamana na mwenyeji Rais wa Jamhuri ya Angola João Manuel Gonçalves Lourenço.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan azindua hospitali ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nchini Angola.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi amezindua Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Luanda, nchini Angola.

Rais Samia ambaye yuko kwenye ziara rasmi nchini Angola, alizindua hospitali hiyo akiwa ameandamana na mwenyeji Rais wa Jamhuri ya Angola João Manuel Gonçalves Lourenço.

Kupitia ukurasa wake wa X, Samia alisema hospitali hiyo imepewa jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa heshima ya mchango mkubwa wa Rais huyo wa kwanza wa Tanzania, katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, hususan kwenye nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Angola.

Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Luanda, nchini Angola.

“Heshima hii kubwa kwa Taifa letu ni kielelezo cha uhusiano wa kihistoria na urafiki wa kudumu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa katika mshikamano wa kupigania uhuru, na unaoendelea kuimarishwa kupitia ushirikiano wa kiuchumi kwa maendeleo ya watu wetu,” alisema Rais Samia.

Hospitali hiyo ya kisasa, iliyopo katika eneo la Kilamba jijini Luanda, inatarajiwa kuwa miongoni mwa hospitali za kisasa zaidi nchini Angola, ikiwa na uwezo wa kuhudumia mamia ya wagonjwa kwa wakati mmoja kupitia vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba, vyumba vya upasuaji, huduma za wagonjwa mahututi (ICU), kitengo maalumu cha wagonjwa wa majeraha ya moto, maabara za kisasa, huduma za ukarabati wa afya pamoja na miundombinu ya mafunzo na utafiti wa kitabibu.

Share This Article