EACC yaelezea wasiwasi kuhusu watumishi wa umma wanaojihusisha kwenye siasa

KBC Digital News
1 Min Read
Abdi Mohamud, Mkurugenzi Mkuu, EACC

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC), imeelezea wasiwasi wake kuhusiana na kujihusisha kwa watumishi wa umma kwenye kampeni za kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Tume hiyo imeonya kwamba hatua ya maafisa wa serikali kujihusisha na siasa inaweza kusababisha ukiukaji wa sheria na hali ya kutojali pamoja na ukosefu wa usawa kwenye safu za kisiasa.

Huku ikisema sheria ya uongozi na uadilifu inawapa nafasi mawaziri kujihusisha na siasa, tume ya EACC imesema maafisa wengine wa serikali, hasa makatibu, hawafai kuegemea upande wowote wa kisiasa.

Akizungumza kwenye msitu wa Karura kufuatia kutwaliwa kwa kipande cha ardhi cha ekari 17.5 cha thamani ya shillingi bilioni 2.8, mkurugenzi mkuu wa tume ya EACC,  Abdi Mohammud, alithibitisha kwamba tume hiyo inachunguza madai ya jaribio la wastawishaji wa kibinafsi kunyakua eneo moja la msitu wa Ngong.

Aidha, Mohammud alisema pamoja na kukamatwa kwa washukiwa 11 wanaohusishwa na ubadhirifu wa shilingi Milioni 85 kutoka kwa hazina ya serikali ya kitaifa ya ustawi wa eneo bunge la Eldama Ravine, tume hiyo pia inachunguza hazina nyinginezo ambako wabunge na wanachama wa bodi wanadaiwa kutumia vibaya pesa za umma.

Share This Article