Wanafunzi wa Egerton wapanda miche 200,000 kuokoa msitu wa Baraget

Msitu wa Baraget ni sehemu ya msitu wa Mau, ambao ni chanzo muhimu cha mito Molo na Njoro.

KBC Digital News
2 Min Read
Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Egerton washiriki upanzi wa miche 200,000 kaunti ya Nakuru.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton, kwa ushirikiano na kundi la vijana la Youths for Green Action Kenya, wameanzisha zoezi la upanzi wa miche 200,000 katika msitu wa Baraget, Kaunti ya Nakuru.

lengo kuu la zoezi hilo ni kurejesha msitu huo uliodhoofika katika hali yake ya awali, na hivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, msimamizi wa kundi hilo, Dennis Asiya, alisema juhudi hizo zinalenga kurejesha mfumo ikolojia wa msitu huo ambao umeathiriwa pakubwa na shughuli za kibinadamu, hususan ukataji miti ovyo.

Aliongeza kuwa uharibifu huo umechangia pakubwa kukauka kwa vyanzo vya mito, hali inayowaathiri wakazi wanaotegemea maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo na mifugo.

Msitu wa Baraget ni sehemu ya msitu wa Mau, ambao ni chanzo muhimu cha mito Molo na Njoro, hivyo kuufanya kuwa na umuhimu mkubwa wa kiikolojia. Aidha, amebainisha kuwa upandaji miti utachangia kuongeza kiwango cha mvua katika eneo hilo.

Kundi hilo la vijana, kwa ushirikiano na Huduma  ya Misitu ya Kenya (KFS), linapania kupanda miche hiyo kwa awamu nne.

Afisa wa KFS katika Kaunti ya Nakuru, Bena Ngenywa, amewataka wakazi kushirikiana katika kulinda miche hiyo ili kuhakikisha inamea na kukua ipasavyo, kwa lengo la kufanikisha asilimia 30 ya msitu huo katika kaunti hiyo.

Wanafunzi walioshiriki zoezi hilo wamesema shughuli hiyo itawapa fursa ya kupata tajriba katika masuala ya uhifadhi wa mazingira.

Share This Article