Kamishna wa IEBC aelezea hofu juu ya vurugu za kisiasa kuelekea 2027

radiotaifa
1 Min Read
Dkt. Alutalala Mukhwana - Kamishna wa IEBC

Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Dkt. Alutalala Mukhwana, ameelezea hofu kwamba uchaguzi mkuu ujao huenda usiakisi matakwa ya Wakenya iwapo vurugu za kisiasa zitaendelea kulitikisa taifa.

Dkt. Mukhwana amesema kuwa machafuko yanayochochewa kisiasa, yasipodhibitiwa, yataathiri matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2027.

Akizungumza mjini Kitale wakati wa ufunguzi wa tamasha la siku mbili la Majadiliano ya Wananchi, kamishna huyo alisema kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotekelezwa na makundi ya wahuni kwa misingi ya kisiasa vinazua hofu miongoni mwa wapiga kura, hasa wanawake.

Majadiliano hayo yanayowalenga vijana yameandaliwa na IEBC kwa ushirikiano na Kituo cha Demokrasia ya Vyama Vingi (CMD-Kenya).

Aliwashutumu wanasiasa kwa kuwasajili na kuwafadhili vijana ili kuzua vurugu kwa lengo la kujipatia ubabe wa kisiasa, akisema kuwa hali hiyo ina athari kubwa kwa uchaguzi mkuu ujao.

Taarifa ya Joseph Mwanjala 

Share This Article