Washukiwa watatu wakamatwa kwa wizi wa shilingi milioni 22

Washukiwa hao walitumia mbinu za teknolojia kuhitilafiana na mifumo ya fedha ya kidijitali ya chama hicho cha akiba na mikopo, kupora fedha hizo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa watatu wakamatwa kwa wizi wa shilingi milioni 22.

Maafisa wa polisi katika eneo la Imenti Kaskazini kaunti ya Meru, wamewakamata washukiwa watatu wanaodaiwa kuipora chama cha ushirika cha akiba na mikopo shilingi milioni 22.4.

Kulingana na maafisa hao, washukiwa hao walitumia mbinu za teknolojia kuhitilafiana na mifumo ya fedha ya kidijitali ya chama hicho cha akiba na mikopo, kupora fedha hizo.

Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema ilibainisha kuwa Allan Karani ambaye ni afisa msaidizi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), alipanga njama hiyo ya uhalifu, huku uchunguzi zaidi ukiwaelekeza makachero hao kwa  Tony Mwenda, Sharon Kendi, Brivin Dentel, na Mawingu Plus Ltd, ambao akaunti zao zilitumika kwa uporaji huo.

Mnamo Juni 4,2026, maafisa hao walimkamata Tony Mwenda, huku makahakama ikiagiza azuiliwe. Juni  10, 2026, washirika wake Allan Karani, Betty Kanana, na Sharon Kendi, walikamatwa wakiwa na simu za rununu na tarakilishi ya kampuni ambazo kwa sasa zinachunguzwa na maafisa wa polisi.

Kwa sasa washukiwa hao wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani.

“Maafisa wa DCI wamejitolea kulinda maslahi ya umma na wale wanaopatikana na hatia, wanawajibishwa kikamilifu kupitia sheria,” ilisema DCI.

Share This Article