Wafanyakazi wa sekta ya ukarimu katika Kaunti ya Bungoma ambao hawana vyeti rasmi za kitaaluma lakini wamepata uzoefu wa vitendo kazini wamehimizwa kutumia fursa ya mpango wa mafunzo unaofadhiliwa na serikali.
Mpango huo unanuiwa kuwawezesha kupata vyeti vya kitaaluma kupitia Utambuzi wa Ujuzi Uliopatikana Awali, RPL.
Mpango huo wa siku 14, unaofadhiliwa na hazina ya utalii ya serikali kuu, umezinduliwa katika chuo cha kitaifa cha Ufundi cha Bungoma ukiwalenga wafanyakazi wa sekta ya ukarimu kwa kuwapa fursa ya kutathminiwa rasmi ujuzi na uzoefu walioupata kazini na kutunukiwa vyeti vinavyotambuliwa.
Mpango huo unalenga kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya utalii na ukarimu, huku ukiimarisha ushindani wa wafanyakazi wenye ujuzi katika soko la ajira.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Kaunti ya Bungoma anayeshughulikia Utalii, Nicholas Kiboi, alisema kuwa mpango wa RPL unatoa njia muhimu ya kutambua umahiri unaopatikana kupitia uzoefu wa kazi.
Alisema mpango huo unawawezesha wafanyakazi kupata sifa zinazotambuliwa kitaifa bila kulazimika kuanza mafunzo rasmi kutoka mwanzo.
Naibu Mkuu wa taasisi hiyo ya Bungoma, Charles Lumuli, alisema programu hiyo itaziba pengo kati ya uzoefu wa vitendo na sifa za kitaaluma, hivyo kuwapa washiriki fursa kubwa zaidi za maendeleo ya taaluma na ajira.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wadau wa Sekta ya Utalii na Ukarimu chini ya Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Viwanda Kenya William Ouya, aliwahimiza wafanyakazi wa sekta ya ukarimu na wakazi kushiriki kwa wingi.