Rais William Ruto amemteua Charles Owino Wahong’o kuwa msemaji mpya wa serikali kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika uongozi wa juu serikalini yaliyotangazwa Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Owino amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali hadi Afisi ya Rais.
Atahudumu kama Kaimu Mkuu wa Mawasiliano ya Serikali na pia Msemaji wa Serikali.
Wakati huo huo, Isaac Mwaura amepandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Uanuwai, Ushirikishwaji na Haki za Watu Walemavu katika Afisi ya Rais, hivyo kuhitimisha kipindi chake kama Msemaji wa Serikali.
Mabadiliko hayo ni sehemu ya uteuzi mpana wa Rais na upangaji upya wa watumishi wa umma ulioidhinishwa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Aidha, Rais Ruto amewasilisha majina kadhaa bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa, akiwemo Dkt. Duncan Ojwang Oburu aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi, IPOA, Antonina Lentoijoni na Wilson Sossion walioteuliwa kuwa makamishna wa Tume ya Kuajiri Walimu,TSC na Flora Mutua aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, PSC.
Vilevile, watu saba wameteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Kiufundi ya Mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Kaunti,IGRTC, uteuzi unaosubiri kuidhinishwa katika kikao cha uratibu wa Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti.