Kenya na Marekani zinaunga mkono mchakato wa kuleta amani Sudan, asema Mudavadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya na Marekani zimejitolea kuhakikisha amani nchini Sudan.

Kenya na Marekani zimejitolea kuleta amani na udhabiti  nchini Sudan, kulingana na Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Alipokutana na ujumbe kutoka Marekani ukiongozwa na Peter Lord ambaye ni naibu waziri anayeshughulikia Afrika Mashariki, Sudan na Sudan Kusini pembezoni mwa mkutano wa London–Sudan katika jumba la Lancaster,  Mudavadi alidokeza kuwa nchi hizo mbili zinajizatiti kuharakisha mchakato wa kuleta amani nchini Sudan na zinaunga mkono juhudi za kuhakikisha Sudan iliyo moja.

“Marekani ilitambua jukumu la Kenya katika kupigia debe upatikanaji amani katika kanda hii, hususan katika eneo la Maziwa Makuu na kurejelea uungaji wake mkono wa juhudi zinazoendlea za kuleta amani Sudan,” alisema Mudavadi.

Katika mkutano huo, Mudavadi alikuwa ameandamana na mwanasheria mkuu Dorcas Oduor, mshauri wa kitaifa kuhusu usalama balozi  Monica Juma na balozi Catherine Karembu.

Mudavadi ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Nje, anahudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa serikali ya Uingereza.

Waziri huyo anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Kenya kuhusu amani na usalama wa kanda ya Maziwa Makuu, hususan kuhusu mzozo nchini Sudan ambao hadi sasa umedumu miaka mitatu.

Mzozo huo wa Sudan umesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao, wakiwemo kina mama na watoto.

Website |  + posts
Share This Article