Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani, ameihakikishia Jamii ya Waislamu katika Kaunti hiyo kuwa ardhi ya Msikiti mkongwe wa Kongo, Diani, eneo bunge la Msambweni haitanyakuliwa.
Achani alisema ili kuzuia unyakuzi wa ardhi hiyo, serikali yake imeweka vikwazo vya kuzuia uuzaji wa ardhi hiyo.
Kauli ya Gavana huyo inajiri baada ya taarifa kusambaa mitandaoni pamoja na vyombo vya habari, kuhusu mabwenyenye wawili waliochapisha tangazo la kuwa na nia ya kuuza ardhi hio yenye ya ekari 18.
Hadi kufikia sasa serikali ya Kaunti ya Kwale kwa ushirikiano na tume ya kitaifa ya ardhi (NLC) na Tume ya kupambana na Ufisadi Nchini (EACC), imefanikiwa kurejesha ardhi mbalimbali zilizonyakuliwa kinyume na sheria, ikiwemo ardhi ya kisiwa cha Kisite Mpunguti, Chale, Lungalunga pamoja na ardhi mbili zilizonyakuliwa katika fuo za bahari huko Diani .
Akizungumza katika halfa ya mashindano ya Quran katika kijiji cha chitsanga huko Tiwi eneo la Matuga, Achani alisema serikali yake haitaruhusu unyakuzi wa ardhi kuendelea katika Kaunti hio, akisema uongozi wake utahakikisha ardhi zote zilizonyakuliwa zinarudishwa kwa wamiliki halali wa ardhi hizo.
Aidha Achani alisema kuwa Serikali ya Kaunti ya Kwale iko na nia ya kutumia ardhi ya Msikiti huo wa Kongo kutengeneza sehemu maalum ya Kidini, huku tayari serikali hio ikifanikiwa kuboresha miundo msingi ya barabara zinazoelekea eneo hilo