Baraza la Magavana limetoa wito kwa bunge la taifa liharakishe mchakato wa kupitisha mswada wa nyongeza ya ufadhili wa serikali za kaunti wa mwaka 2025.
Kulingana na Magavana hao, serikali za kaunti zimekumbwa na changamoto katika kuwahudumia wananchi, kutokana na kuchelewa kupitishwa kwa mswada huo.
Walipofika mbele ya kamati ya bunge la taifa kuhusu ugavi inayoongozwa na Samuel Atandi ambaye ni mbunge wa Alego Usonga, wawakilishi wa Baraza la Magavana Fernandes Barasa wa Kakamega na mwenzake wa Homa Bay Gladys Wanga, waliunga mkono mswada huo jinsi ulivyo, ambao unapendekeza nyongeza ya shilingi bilioni 50.5 kwa ufadhili wa kaunti.
“Mswada huo uliofanyiwa marekebisho, unarejesha ugavi wa mapato jinsi ulivyokuwa kwenye bajeti awali, tunapongeza swala hili,” alisema Gavana Barasa.
Barasa alidokeza kuwa mswada kuhusu nyongeza ya ugavi kwa serikali za kaunti, umekuwepo tangu mwaka wa kifedha wa 2021/2022.
Kwa upande wake, Gavana Wanga alielezea wasiwasi kuhusu kutenganishwa kwa mswada wa nyongeza kuhusu ugavi kutoka kwa sheria ya ugavi wa mapato kwa kaunti(CARA), hatua aliyosema imechangia kucheleshwa kutumwa kwa fedha katika kaunti.
“Nyongeza hizi awali zilikuwa sehemu ya mpango wa CARA. Tunapendekeza mfumo huo urejeshwe,” alisema Wanga.
Atandi aliwahakikishia Magavana hao kwamba, kamati hiyo imejitolea kuharakisha kupitishwa kwa mswada huo.