Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amekanusha madai kwamba serikali ilipokea msaada wa mbolea kutoka Urusi.
Kulingana na Dkt. Ronoh, Kenya ilipokea tu mali ghafi inayotumika kutengeza mbolea kutoka Russia.
Akizungumza wakati wa mkutano kuhusu mfumo wa kitaifa wa chakula katika hoteli moja Jijini Nairobi, Dkt. Ronoh alidokeza kuwa baada ya kupokea mali ghafi, Kenya iligharamia utayarishaji wa mbolea hiyo kwa kununua mali ghafi zaidi iliyohitajika kwa utengezaji wa mbolea.
Kwa mujibu wa Katibu huyo wa kilimo, serikali ilipokea tani 34,000 za kemikali ya utayarishaji wa mbolea na wala sio mbolea yenyewe.
Aliongeza kuwa gharama ya utayarishaji mbolea hiyo ililipiwa na wakulima licha ya msaada huo kufuatia ununuzi wa mali ghafi nyingine iliyohitajika kutayarisha mbolea hiyo.