Maafisa wa polisi wamemkamata wakili mwenye makao yake Jijini Nairobi, kwa madai ya kuhusika katika ulaghai wa ardhi.
Abdulahi Musdaf Hussein, anadaiwa kwamba alijaribu kumiliki ardhi ambayo haikuwa yake.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ilisema kuwa, mlalamishi ambaye ni mmiliki halali wa ardhi hiyo alipokea agizo la mahakama lililoashiria Musdaf ndiye mmiliki wa ardhi yake.
Baada ya kupokea malalamishi, maafisa wa DCI walianza uchunguzi mara moja uliobainisha kuwa wakili huyo alikuwa na stakabadhi bandia za umiliki wa ardhi hiyo.
Musdaf alikamatwa katikati mwa jiji la Nairobi na kuzuiliwa kwenye korokoro za polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.