Chongqing yaweka mawasiliano ya umma mbele katika utawala wa jiji

Mfumo wa mawasiliano wa Chongqing waunganisha serikali, vyombo vya habari na wananchi katika utungaji na utekelezaji wa sera.

KBC Digital News
5 Min Read

CHONGQING, China – Serikali ya Chongqing imeeleza jinsi mawasiliano ya umma yanavyoweza kuboresha utawala wa miji mikubwa kwa kuongeza uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na ufanisi wa utekelezaji wa sera.

Akizungumza katika ufunguzi wa mjadala wa nne wa wasemaji wa serikali wa China na nchi za ulaya ya kati na mashariki (China–CEEC) uliofanyika karibuni, Naibu Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati ya Manispaa ya CPC Chongqing na Msemaji wa Serikali ya Manispaa ya Chongqing, Zhang Qiong, alisema mikutano na waandishi wa habari inapaswa kuwa zaidi ya kutoa taarifa za serikali.

Alisema mawasiliano yanapaswa kuanza kabla ya sera kutekelezwa kwa kuwashirikisha wananchi, kupokea maoni yao na kuhakikisha kuna mrejesho wa mara kwa mara katika mchakato mzima wa utungaji na utekelezaji wa sera.

Kwa mujibu wa Zhang, mfumo huo hupunguza kutokuelewana kuhusu sera, huimarisha ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya habari na wananchi, na kufanya utawala wa miji mikubwa kuwa wazi zaidi na unaotabirika.

Alisema utawala wa kisasa unahitaji kuweka uwiano kati ya maamuzi ya kitaalamu na uelewa wa wananchi, huku mikutano na waandishi wa habari ikibaki daraja muhimu linalounganisha serikali na jamii.

Akitumia Chongqing kama mfano, Zhang alisema jiji hilo lina eneo la kilomita za mraba 82,400 na wakazi wa kudumu wapatao milioni 33, hali inayohitaji mfumo madhubuti wa utawala kutokana na ukubwa wake, muundo wake changamani na mahitaji tofauti ya wananchi.

Alibainisha kuwa mtindo wa zamani wa mawasiliano uliolenga kutoa taarifa pekee bila ushirikishwaji wa wananchi hauwezi tena kukidhi mahitaji ya sasa, kwani unaweza kusababisha tafsiri potofu za sera, matarajio yasiyoendana na utekelezaji dhaifu.

Kutokana na hali hiyo, Chongqing imebadili mfumo wake wa utoaji wa taarifa kutoka kueleza sera baada ya maamuzi kufanyika kwenda kuwashirikisha wananchi katika kila hatua ya mchakato. Serikali hiyo pia imehamisha msisitizo kutoka kusambaza taarifa pekee hadi kutumia mawasiliano kama sehemu ya kuboresha utawala.

Zhang alisema Chongqing imeanzisha mfumo wa pamoja wa kupanga ajenda za mikutano na waandishi wa habari ambapo idara za serikali hubaini masuala muhimu ya utawala, vyombo vya habari huwasilisha hoja zinazogusa wananchi, huku majukwaa ya kidijitali yakikusanya maoni ya umma. Ofisi ya habari ya serikali ya manispaa hufanya tathmini ya pamoja kabla ya kuamua ajenda za kutolewa kwa umma.

Alitaja marekebisho ya nauli za metro yaliyofanyika mwaka jana kuwa mfano wa mafanikio ya mfumo huo. Serikali ilitoa maelezo mapema kuhusu sababu za sera hiyo na manufaa yake kwa wananchi, hatua iliyosaidia kupunguza upotoshaji na kuongeza uelewa wa umma.

Kwa mujibu wa Zhang, Chongqing pia imeimarisha ushiriki wa wananchi kwa kutumia njia za mtandaoni na ana kwa ana. Kabla ya mikutano na waandishi wa habari kufanyika, wananchi huwasilisha maswali kupitia mitandao, huku viongozi wa serikali wakijibu hoja muhimu moja kwa moja wakati wa mikutano hiyo.

Kati ya mwaka 2024 na 2025, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Manispaa ya Chongqing iliandaa karibu mikutano 300 na waandishi wa habari, ikijibu maswali 1,433 kutoka kwa wanahabari na maswali 1,512 kutoka kwa wananchi.

Aidha, serikali imeanzisha mfumo wa kufuatilia maoni ya wananchi kuanzia ukusanyaji wa hoja, uchambuzi, ugawaji wa majukumu, ufuatiliaji hadi tathmini ya matokeo. Mfumo huo umewezesha kutatua zaidi ya changamoto 4,500 zinazohusu maisha ya wananchi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Zhang alisema uzoefu wa Chongqing unaonyesha kuwa mikutano na waandishi wa habari si chombo cha mawasiliano pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga maridhiano, kutatua changamoto za utawala na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aliongeza kuwa Chongqing pia imeimarisha mawasiliano ya kimataifa kupitia taasisi maalumu ya mawasiliano, ikitumia lugha na mbinu zinazorahisisha hadhira ya kimataifa kuelewa maendeleo ya jiji hilo. Kwa sasa, Chongqing inaendesha tovuti ya iChongqing yenye takribani watumiaji milioni 23 kutoka nje ya China pamoja na programu ya Bridging News.

Akihitimisha hotuba yake, Zhang aliwahimiza washiriki wa mkutano kutembelea Chongqing ili kujionea maendeleo, ubunifu na mvuto wa jiji hilo la kisasa.

Hisani/ iChongqing.info

Share This Article