Upinzani wa Julai 15 hauna kifani katika historia ya demokrasia duniani – Erdogan

Rais anasema hatua kubwa imepigwa kuelekea mustakabali wenye ustawi zaidi huku Uturuki ukiimarisha demokrasia, usalama, na maendeleo ya kitaifa

KBC Digital News
3 Min Read
Recep Tayyip Erdoğan ni Rais wa Jamhuri ya Uturuki.

Miaka kumi iliyopita, tarehe 15 Julai 2016, Uturuki ilikabiliwa na moja ya majaribio makali zaidi ya mapinduzi ya kijeshi katika historia yake ya kisiasa. Rais Recep Tayyip Erdoğan anasema jaribio hilo, lilipangwa na mtandao wa kigaidi uliokuwa umejipenyeza ndani ya taasisi za dola, na lilikusudia kuitumbukiza nchi katika machafuko na kudhibiti mustakabali wake.

Rais Erdoğan anaeleza kuwa raia wa Uturuki, kwa kusimama imara kutetea uhuru na mustakabali wao, walionyesha ulimwengu kuwa nia ya wananchi haiwezi kutawaliwa kwa nguvu. Anasema busara, ujasiri, na uwezo wa kuona mbali uliooneshwa na taifa lake usiku huo hauna mfano katika historia ya demokrasia duniani.

Anaeleza kuwa jaribio hilo la mapinduzi, lililoendeshwa na kile kinachoitwa “shirika la kigaidi la Fetullah (FETO),” halikuwa jaribio la kawaida la mapinduzi, bali ni shambulio kamili dhidi ya uhuru wa nchi, kwani likilenga taasisi muhimu kama Ikulu na Bunge la Kitaifa.

Erdoğan anakumbuka kuwa usiku huo alisisitiza kutokuwa na imani na mamlaka yoyote iliyo kuu kuliko wananchi wenyewe, na kwamba wananchi walijibu wito huo kwa kutoka mitaani bila kuyumba, wakikataa kutawaliwa na shirika hilo la kigaidi.

Baada ya tukio hilo, serikali ilianzisha mageuzi makubwa ya kimuundo kuondoa mitandao inayopinga demokrasia ndani ya taasisi za dola, na kufanya operesheni za ndani na nje ya nchi dhidi ya makundi ya kigaidi.

Hatimaye, mpango wa “Uturuki Isiyo na Ugaidi” ulizinduliwa kama sehemu ya dira ya “Karne ya Uturuki.”

Kiuchumi na kimaendeleo, Erdoğan anaeleza mafanikio katika sekta za nishati, usafiri, afya, kilimo, teknolojia, na ulinzi, akitaja bidhaa za kitaifa kama gari la umeme la TOGG, ndege ya kivita ya KAAN, meli za kivita, na ndege zisizo na rubani.

Kidiplomasia, anasema Uturuki imekuwa mwanachama muhimu katika kutatua migogoro ya kikanda na kimataifa, ikisimama upande wa waliokandamizwa badala ya wenye nguvu.

Rais huyo anasisitiza umuhimu wa kuendelea kupambana na kundi la FETO duniani kote, akikumbuka raia 253 waliouawa kupitia mapinduzi usiku huo wa Julai 15, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono mapambano ya Uturuki dhidi ya ugaidi.

Recep Tayyip Erdoğan ni Rais wa Jamhuri ya Uturuki

Share This Article