Mageuzi ya uchumi Chongqing yachukua mkondo wa uzalishaji na biashara

KBC Digital News
3 Min Read

Mji wa Chongqing umebadilisha mkakati wake wa ukuaji kutoka utegemezi wa ardhi na miundombinu na kuukumbatia sekta viwanda vya kisasa na njia za usafirishaji kama vichocheo vipya za uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya mwaka 2025 iliyotolewa na ofisi ya takwimu ya jiji hilo, pato la taifa la Chongqing lilivuka yuan trilioni 3.3 (takribani dola bilioni 477.4 za Marekani), ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.3 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Ingawa ukuaji huo unaonekana kuwa thabiti, takwimu zinaonesha mabadiliko makubwa ya kimuundo. Jumla ya uwekezaji wa mali za kudumu ilipungua kwa asilimia 0.7, hali inayoashiria kuwa vyanzo vya ukuaji wa uchumi vimebadilika.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja, ukuaji wa Chongqing ulitegemea mifumo miwili mikuu, zikiwemo ufadhili wa miundombinu unaotegemea ardhi, pamoja na sekta ya utengenezaji wa kompyuta hasa tarakilishi, iliyotegemea gharama nafuu za uzalishaji.

Hata hivyo, mwaka 2025 kulionekana kuwa na changamoto ambapo nguzo hizi mbili zilianza kudorora. Uwekezaji katika sekta ya mali isiyohamishika ulipungua kwa asilimia 14.7, sekta ya ujenzi ikashuka kwa asilimia 1.1, huku utengenezaji wa kompyuta na vifaa vya kielektroniki ukishuka kwa asilimia 4.4.

Wakati huo huo, uwekezaji katika sekta ya viwanda uliongezeka kwa asilimia 8.5, na ule wa maboresho ya teknolojia ya viwanda kupanda kwa asilimia 19.2, ukionesha mwelekeo mpya wa mitaji hadi uzalishaji wa kisasa.

Sekta ya viwanda pia ilionekana kuimarika, ambapo thamani ya uzalishaji kwa makampuni makubwa iliongezeka kwa asilimia 5.9. Sekta ya magari ya nishati mpya iliongoza kwa ukuaji wa asilimia 17 kwa thamani na asilimia 36 katika uzalishaji.

Aidha, njia za usafirishaji zilichangia kwa kiasi kikubwa, ambapo korido mpya ya biashara ya kimataifa ya nchi kavu na bahari,  yaani the New International Land-Sea Trade Corridor, ilirekodi ongezeko la asilimia 30 ya makontena na asilimia 25 ya thamani ya mizigo.

Licha ya mafanikio hayo, faida za viwanda zilipungua kwa asilimia 3.7, huku sekta ya utengenezaji ikishuka kwa asilimia 4.7, jambo linaloashiria ushindani mkali sokoni.

Mabadiliko haya pia yameathiri matumizi ya wananchi. Mapato ya mtu mmoja mmoja yaliongezeka kwa asilimia 4.7, lakini matumizi yakapanda kwa asilimia 2.2 tu, huku faharasa ya bei za watumiaji ikiongezeka kwa asilimia 0.1.

Hii inaashiria kuwa kadri faida za sekta ya mali isiyohamishika zinavyozidi kupungua, wananchi wanakuwa waangalifu zaidi katika matumizi yao.

Kwa ujumla, mji wa Chongqing inaingia katika awamu mpya ya ukuaji wa uchumi unaotegemea uzalishaji halisi badala ya kutegemea ule wa mali na mikopo.

Makala kwa Hisani ya iChongqing.info

Share This Article