Rais William Ruto jana Jumamosi Aprili 18, 2026 alikuwa katika kaunti ya Mandera ambapo alihudhuria hafla mbili na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo.
Alitangulia kuhudhuria mkutano uliolenga kuwezesha kina mama kiuchumi katika uwanja wa michezo wa Mandera ambapo alipokelewa na viongozi kadhaa wa eneo hilo.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, kiongozi wa nchi aliahidi kwamba eneo hilo halitasalia nyuma kimaendeleo kwani lmejumuishwa katika ajenda ya maendeleo ya serikali ya kitaifa.
Kiongozi wa taifa alisema miradi muhimu ya miundo msingi inaendelea kutekelezwa ili kuimarisha uchukuzi na uchumi wa eneo hilo, akiangazia ujenzi wa barabara kuu ya kutoka Isiolo hadi Mandera aliyoitaja kuwa kiunganishi muhimu cha kaskazini mwa kenya.
Rais Ruto alisema pia kwamba serikali inapanga kuajiri walimu 1,800 kutoka eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya chini ya mpango unaokusudiwa kuhakikisha usawa kote nchini.
Baada ya mkutano huo, Rais alizuru mradi wa maji wa Banissa na ule wa soko la kisasa la Banissa kabla ya kuhudhuria hafla ya kutoa shukrani ya mbunge wa eneo la Banissa, Ahmaed Hassan.
Katika hafla hiyo Rais alisisitiza kwamba umoja wa wakenya ndio nguvu ya nchi ambayo ni msingi wa uthabiti, maendeleo na mustakabali wa taifa ndiposa ipo haja ya kukataa wanaozua migawanyko.
Kulingana naye, serikali inashirikiana na viongozi wote kote nchini ili kufanikisha ajenda ya maendeleo.