Hazina Kuu kuwasilisha bajeti ya shilingi trilioni 4.8

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Fedha na Mipango ya Taifa, John Mbadi.

Waziri wa Fedha na Mipango ya Taifa John Mbadi, leo Alhamisi anatarajiwa kuwasilisha makadirio ya matumizi ya pesa za serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 ya shilingi trilioni 4.8 katika majengo ya bunge.

Bajeti hiyo inajiri wakati ambapo taifa hili linashuhudia ongezeko la mfumko wa bei kwa asilimi 6.7,  ongezeko hilo likidaiwa kusababishwa na bei za juu za bidhaa za petroli.

Kwenye bajeti hiyo, serikali inalenga kutenga shilingi trilioni 1.5 kwa hazina ya pamoja ya utoaji huduma, ambayo awali ilikuwa imetengewa shilingi trilioni 1.37.

Kwenye kitita hicho cha shilingi trilioni 4.8, serikali za kaunti zinatarajiwa kupokea mgao wa shilingi bilioni 428 ikiwa ni pamoja na ruzuku.

Akizungumza alipowasili afisini mwake Alhamisi asubuhi, Mbadi alikiri kuwepo kwa changamoto, huku serikali ikijizatiti kuziba mianya na kuimarisha uzingatiaji sheria.

Aidha, katika bajeti hiyo mpato ya taifa ikiwa ni pamoja na ruzuku, zinatarajiwa kuongezeka kwa shilingi trilioni 3.67.

Waziri Mbadi, hata hivyo, amewahakikishia wakenya kuwa bajeti hiyo haina vipengee fiche,  akisema kuwa makisio yaliwasilishwa kwa umma kuanzia tarehe 30, mwezi Aprili, mwaka huu.

Mataifa mengine ya Afrika mashariki pia yanatarajiwa kuwasilisha bajeti zao, huku Rwanda ikitarajiwa kutangaza bajeti ya dola bilioni 5.4  ambayo ni ongezeko la asilimia 12% kutoka kwa bajeti ya mwaka uliopita ya dola 4.8 bilioni.

Bajeti hiyo inatarajiwa kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Rwanda, na asilimia 68 inatarajiwa kufadhiliwa na mapato ya ndani.

Share This Article