Maafisa wa kituo cha Polisi cha Keringet kuhamishwa

Murkomen pia alitangaza kupelekwa kwa kikosi maalumu cha polisi katika eneo hilo ili kuimarisha misako ya kiusalama, kama sehemu ya juhudi mpya za kukabiliana na uraibu wa mihadarati.

Tom Mathinji
2 Min Read
Kipchumba Murkomen - Waziri wa Usalama wa Taifa.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ameagiza kuhamishwa mara moja kwa Maafisa wote wa Polisi wanaohudumu katika Kituo cha Polisi cha Keringet, kaunti ya Nakuru.

Kwenye mkutano wa umma ulioandaliwa eneo la Keringet kaunti ya Nakuru, waziri huyo aliagiza maafisa ambao wamehudumu katika kituo hicho kwa muda mrefu na wanaohusishwa na uraibu wa pombe wahamishwe, wasajiliwe katika mipango ya urekebishaji tabia na wachukuliwe hatua za kinidhamu.

“Maafisa wote ambao wamehudumu hapa kwa muda mrefu na ambao wanaathiriwa na uraibu wa pombe, watawekwa kwenye mpango wa urekebishaji tabia na wachukuliwe hatua za kinidhamu. Maafisa wapya 20 wa Polisi wataletwa hapa,” alisema Murkomen katika mkutano huo.

Murkomen pia alitangaza kupelekwa kwa kikosi maalumu cha polisi katika eneo hilo ili kuimarisha misako ya kiusalama, kama sehemu ya juhudi mpya za kukabiliana na uraibu wa mihadarati katika eneo hilo.

“Tumekubaliana kwamba kundi maalum la maafisa wa usalama litaletwa hapa kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati,” aliongeza waziri huyo.

Aidha, aliwaonya walanguzi mihadarati katika eneo hilo na kote nchini, akisema serikali itaimarisha msako dhidi ya biashara hiyo haramu.

Wakati huo huo aliwatahadharisha maafisa wa usalama na wale wa utawala katika maeneo mbalimbali dhidi ya kushirikiana na wahalifu, akisisitiza kuwa yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, ambaye aliandamana na waziri Murkomen, alimwelekeza kamanda wa polisi wa eneo hilo, Samuel Ndanyi, kuongoza msako mpya wa kuondoa pombe haramu, dawa za kulevya na shughuli nyingine za uhalifu katika eneo hilo.

Share This Article