Kituo cha kuwatenga wagonjwa chabuniwa katika uwanja wa JKIA

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya yabuni kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola JKIA.

Kenya inazidi kuimarisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola pamoja na changamoto zingine za afya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), kwa lengo la kuimarisha ugunduaji wa mapema na kufanikisha usalama wa afya ya umma.

Katibu katika Idara ya Afya ya Umma na Ubora wa viwango vya Utaalam Mary Muthoni, siku ya Jumamosi alifanya ziara ya ukaguzi katika uwanja wa JKIA, kukadiria mikakati ya kuzuia msambao wa ugonjwa huo hatari hapa nchini.

Ziara hiyo iliangazia taratibu za kuwachunguza wasafiri, vituo vya kuwatenga wagonjwa, utayari wa maabara pamoja na mikakati ya kushughulikia dharura.

Kitengo cha usimamizi cha mipakani kilicho na makao yake katika uwanja huo wa ndege, kimeimarisha uchunguzi wa Ebola katika kiingilio nambari 6, hukuu kiingilio nambari 16 kikitengewa wasafiri wanaotoka maeneo yenye hatari kubwa.

“Kiingilio nambari 16 kituo cha kuwatenga wagonjwa kinachosimamiwa na maafisa wa afya, kimebuniwa iwapo kutaripotiwa kisa chochote,” alisema Muthoni.

Katibu huyo aliwapongeza maafisa wa afya ambao wako mstari wa mbele, kwa kujitolea kwao kulinda afya ya umma, akidokeza kuwa Wizara ya Afya itadumisha mifumo ya kugundua na kukabiliana na hatari za afya ya umma.

Share This Article