Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ameungana na viongozi wengine kuhudhuria kongamano la 17 la ngazi ya juu kuhusu amani, usalama na uthabiti barani Afrika linaloandaliwa nchini Gabon.
Mkutano huo wa siku mbili wenye kaulimbiu kuimarisha Usitishaji wa Vita, Mazungumzo ya Kitaifa na Maridhiano ya amani ya kudumu, umewaleta pamoja wajumbe wa kuleta amani, wanadiplomasia, wabuni sera na wadau wengine.
Kupitia kwa ukurasa wake wa X, Rais huyo mstaafu alisema mkutano huo utapigia kurunzi kuimarisha juhudi za Afrika za kuzuia mizozo, upatanishi na amani ya kudumu barani Afrika.
Aidha kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), pia unawajumuisha wawakilishi kutoa Muungano wa Afrika AU, mashirika ya kikanda, wajumbe wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa zamani wa Afrika ili kubuni mikakati ya kufanikisha upatikanaji wa amani ya kudumu na uthabiti wa Afrika.
Wengine watakaoshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja na Mwenyekiti wa AUC Mahmoud Ali Youssouf, Marais wa zamani Olusegun Obasanjo, Mokgweetsi Masisi, Domitien Ndayizeye, Sahle-Work Zewde na Patrice Emery Trovoada.