Kenya yakaa chonjo dhidi ya Ebola, asema Katibu Kipsang

Hii ni kufuatia mlipuko wa Ebola DRC ambapo watu zaidi ya 100 wamefariki huku mtu mmoja akifariki katika nchi jirani ya Uganda.

Martin Mwanje
2 Min Read
Katibu wa Idara ya Usajili wa Raia na Uhamiaji, Dkt. Belio Kipsang

Serikali imeimarisha uangalizi dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwenye kaunti za mpakani kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC. 

Watu 139 wameuawa DRC huku visa 600 vya ugonjwa huo vikiripotiwa.

Katika nchi jirani ya Uganda, visa viwili vya ugonjwa huo vimeripotiwa huku mtu mmoja akifariki.

Akizungumza mjini Busia baada ya kukutana na maafisa wa utawala wa serikali kuu, Katibu wa Idara ya Usajili wa Raia na Uhamiaji Dkt. Belio Kipsang amewahakikishia Wakenya kwamba nchi hii imekaa macho na kujiandaa ipasavyo kudhibiti msambao unaoweza kutokea wa ugonjwa huo.

Dkt. Kipsang alisema serikali imeimarisha mifumo ya upimaji na ufuatiliaji katika maeneo yote ya kuingia nchini, hasa kwenye mpaka wa Kenya na Uganda ili kulinda afya ya umma na kuhakikisha utambuzi wa haraka wa visa vinavyoshukiwa vya Ebola.

Aidha, Katibu huyo amekariri kujitolea kwa serikali kufanya kazi kwa karibu na maafisa wa afya, uhamiaji na asasi za usalama kuhakikisha kampeni za uangalizi na uhamasishaji wa umma zinafanywa katika maeneo yanayokabiliwa na hatari kubwa.

Jumapili iliyopita, Shirika la Afya Duniani, WHO lilitangaza ugonjwa wa Ebola kuwa dharura ya kimataifa, lakini likadokeza kuwa haujafika kiwango cha janga.

“WHO inakadiria hatari ya ugonjwa huo kuwa ya juu katika kiwango cha taifa na kikanda, lakini ya chini katika kiwango cha kimataifa,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Adhanom Ghebreyesus.

Taarifa hii imechangiwa na Said Abdalla

Share This Article