Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Ongata Rongai

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Ongata Rongai.

Kundi la maafisa kutoka asasi mbalimbali za serikali, limewakamata washukiwa wawili wanaoshukiwa kuhusika katika ulanguzi wa mihadarati katika eneo la Ongata Rongai.

Wawili hao walitiwa nguvuni kwenye operesheni iliyoongozwa na Halmashauri ya Taifa ya Kukabiliana na Mihadarati (NACADA), vikosi maalum vya polisi na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Ongata Rongai.

Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao walifanya msako kwenye nyumba inayoshukiwa kutekeleza shughuli za ulanguzi wa mihadarati, ambapo walipata vipande 43 vinavyoshukiwa kuwa mihadarati, mifuko ya plastiki na mashini mbili za kupima uzani miongoni mwa vitu vingine.

Washukiwa wawili ambao walipatikana kwenye nyumba hiyo walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Ongata Rongai.

Baadaye walisafirishwa hadi kituo cha polisi cha Muthaiga ambako wanazuiliwa wakisubiri kufunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa mihadarati.

Share This Article