Kenya haijanakili kisa chochote cha Ebola, asema Waziri Duale

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Afya Aden Duale.

Waziri wa Afya  Aden Duale amehakikisha kuwa Kenya haijanakili kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola, licha ya kuimarisha uchunguzi kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Kulingana na Duale, wizara yake imeimarisha uchunguzi wa Ebola, mifumo ya dharura na kuweka maafisa wa afya katika hali ya tahadhari kama hatua ya kitaifa ya kujiandaa kukabiliana na chamko la ugonjwa huo hatari.

Kwenye mkutano na wanahabari Ijumaa, Duale alisema watu watatu waliokuwa wametoka nchini DRC waliokuwa wakishukiwa kuugua ugonjwa huo,  walitengwa na kuchunguzwa lakini hawakupatikana na Ebola

Aidha, waziri alionya kuwa Kenya bado inakabiliwa na hatari kutokana na uhusiano mkubwa wa usafiri na biashara na nchi zilizoathirika na kwamba ukaguzi pamoja na ufuatiliaji katika maeneo yote ya kuingia nchini, vikiwemo viwanja vya ndege na mipaka umeimarishwa.

Alisema Kenya imetenga vituo vinne vya kupima Ebola ambavyo ni pamoja na maabara ya kitaifa ya afya ya umma, taasisi za utafiti wa matibabu za Nairobi na Kisumu pamoja na maabara moja maalum inayoweza kupelekwa kwenye maeneo inayohitajika.

Wananchi wametahadharishwa dhidi ya safari ambazo sio za lazima nchini DRC na Uganda na pia katika sehemu za mpakani za mataifa hayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema hadi kufikia sasa, watu 177 wamefariki kutokana na Ebola, huku wengine 750 wakiambukizwa ugonjwa huo.

Hakuna chanjo ambayo imethibitishwa kutibu aina hiyo ya Ebola, huku wanasayansi na watafiti wakijizatiti kutafuta chanjo yake.

Share This Article