Wakenya wahimizwa kupiga jeki juhudi za kuhifadhi mazingira

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya wahimizwa kupiga jeki juhudi za kuhifadhi mazingira.

Naibu Rais Kithure Kindiki, ametoa wito kwa Wakenya kuunga mkono juhudi za serikali za kuhifadhi mazingira, akisema ni wajibu wa kikatiba na jukumu la kimaadili.

Huku akisema kuwa uhifadhi wa mazingira umekitwa kwenye katiba, Naibu huyo Rais aliwahimiza Wakenya kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa mazingira, hatua aliyosema itafaidi pakubwa vizazi vijavyo.

“Tuna jukumu la kikatiba kama taifa, kuhifadhi mazingira,” alisema Kindiki.

Prof. Kindiki alikuwa akizungumza katika eneo la Kapyego, kaunti ya Elgeyo-Marakwet wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango wa kuimarisha na uhifadhi wa mfumo ikolojia wa milima ya   Cherangany (CHERISH), pamoja na kuadhimisha siku ya kimataifa ya bayoanuwai.

Akipongeza mradi huo, Kindiki alisema mpango huo unapiga jeki ajenda ya serikali ya upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032, kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mikakati kama hii itasaidia kuafikia lengo la upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032,” alidokeza Naibu huyo wa Rais.

Share This Article