Polisi wakana kuhusika katika visa vya utekaji nyara

Martin Mwanje
1 Min Read
Muchiri Nyaga - Msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi

Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) imepuuzilia mbali madai yanayowahusisha maafisa wake katika visa mbalimbali vya utekaji nyara vilivyoripotiwa nchini.

Kupitia kwa msemaji wake Muchiri Nyaga, huduma hiyo imetaja madai hayo kuwa yasiyokuwa na msingi.

“Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) imebaini kuwepo kwa madai ya mara kwa mara yanayoenea yakiwahusisha maafisa wake kwa visa vya utekaji nyara,” alilalama Nyaga kwenye taarifa.

“Huduma hiyo inakataa katakata madai hayo. Ni ya uongo, yanapotosha, na hayana ushahidi wowote wa kuaminika.”

NPS imemtaka yeyote aliye na taarifa za kuaminika kuhusu mtu aliyepotea au madai ya utekaji nyara kupiga ripoti kwa kituo cha polisi kilicho karibu naye ili hatua madhubuti zichukuliwe.

Huduma hiyo pia imetoa wito kwa umma, vyombo vya habari, mashirika ya kijamii na washikadau wengine kuthibitisha taarifa za utekaji nyara kabla ya kuzitoa.

Share This Article