Serikali kuajiri walimu wengine 20,000 mwaka huu

Martin Mwanje
1 Min Read

Utawala wa Kenya utaajiri walimu wengine 20,000 mwaka huu.

Hatua hiyo itafanya idadi ya walimu walioajiriwa na utawala wa Kenya Kwanza kuwa zaidi ya 120,000.

Rais William Ruto amesema utawala wake umeajiri walimu zaidi ya 100,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Akihutubia taifa wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka katika kaunti ya Mandera, Ruto amesema serikali imedhamiria kutumia elimu kama chombo cha kuongeza kasi ya ustawi wa nchi.

Amesema serikali imeongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi bilioni 500 mwaka 2022 hadi shilingi za sasa zaidi ya bilioni 702.

“Hiyo ndio maana utawala huu umefanya elimu kuwa siyo tu kipaumbele, lakini msingi wa mustakabali wetu. Hakuna taifa linaweza kuinuka kuzidi maarifa, uwezo, na ujuzi wa raia wake.”

Rais pia amesema serikali imejenga madarasa 23,000 na maabara 1,600 zinajengwa kwa lengo la kuiboresha sekta ya elimu.

Kwa upande mwingine, wanafunzi zaidi ya 850,000 wamesajiliwa katika vituo ya masomo ya kiufundi, TVET ili kupata ujuzi unaohitajika kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

 

 

Share This Article