Rais William Ruto ameomba msahama wakazi wa Kaskazini mwa Kenya, kwa kile alichokitaja kuwa kutengwa na kubaguliwa kwao, hasa wakati wa kutafuta kitambulisho cha taifa.
Akiongoza taifa kuadhimisha sherehe za 63 za Sikukuu ya Madaraka katika kaunti ya Wajir leo Jumatatu, kiongozi wa nchi alitoa msamaha huo kwa niaba ya watu na taifa la Kenya, kwa madhila ambayo wakazi hao wamekumbana nayo kwa muda mrefu wakitafuta stakabadhi hiyo muhimu.
“Ningependa kuwahutubia wakazi wa Kaskazini mwa nchi. Kwa niaba ya watu na taifa la Kenya, naomba msamaha kwa kutengwa kwa muda mrefu.. Poleni sana, ndugu zetu. Haikupaswa kuwa hivyo,” alisema Rais Ruto.
Alisimulia kisa cha Bakaja Ibrahim Osman ambaye alizaliwa Wajir Mashariki katika miaka ya 60, lakini kwa muda mrefu hakuweza kupata kitambulisho cha taifa kutokana na kubaguliwa na wakati mwingine akidhaniwa kuwa mshukiwa.
“Hakuchukuliwa kama raia wa Kenya, lakini kama mshukiwa au raia wa kigeni. Alitumwa kutoka afisi moja hadi nyingine, mwaka mmoja baada ya mwingine,” alidokeza Rais Ruto.
Kulingana na Rais Ruto, katiba ya Kenya inatoa fursa kwa kila Mkenya bila kuzingatia kabila, dini au eneo anakotoka, ana haki ya kulindwa, kupata fursa sawa na kuheshimiwa.
“Ndio maana mwezi Februari 2025, nikiwa hapa katika uwanja wa Orahey Wajir mjini, nilitia saini tangazo la kirais kuhusu usajili na utoaji vitambulisho na hati za kuzaliwa kwa wakazi wa Kaskazini mwa nchi na kaunti zingine za eneo hili, na kumaliza mfumo uliokuwepo wa ubaguzi,” alisema Rais Ruto.
Alisema tangazo hilo limezaa matunda, huku wakazi kama vile like Abdirahman Ali Osman na Maryam Isaak Mohamed, ambao walizaliwa mwaka 2007 katika kaunti ya Wajir, wakiwa miongoni mwa maelfu ya vijana ambao walifikisha umri wa miaka 18 mwaja jana, na wamepata vitambulisho vyao vya taifa.
“Hakuna kuitishwa stakabadhi za ziada, hakuna kubaguliwa, hakuna kudharauliwa, unahitaji tu stakabadhi sahihi. Hivi ndivyo inapaswa kuwa,” aliongeza kiongozi huyo wa taifa.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo haikulenga kuwakaribisha raia wa kigeni kupata stakabadhi hiyo kwa njia za ulaghai.
“Vitambulisho vya taifa vitatolewa tu kwa raia halali wa taifa hili.”