Rwanda yaimarisha juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola / Picha ya awali kwa hisani ya IFRC

Waziri Mkuu wa Rwanda Justin Nsengiyumva amesema, nchi hiyo imeweka hatua mwafaka za kuzuia, kufuatilia na kutibu ugonjwa wa Ebola, iwapo utazuka nchini humo.

Kulingana na Nsengiyumva, Rwanda ina vifaa vinavyohitajika kulinda afya ya umma dhidi ya ugonjwa huo ambao umetajwa kuwa janga la Kimataifa.

Akizungumza na wanahabari, Waziri Mkuu huyo aliwataka raia wa nchi hiyo kuwa watulivu, na katika hali ya tahadhari hususan kwa kuzingatia hali ya juu ya usafi na kuripoti kisa chochote cha kutiliwa shaka.

Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Rwanda Sabin Nsanzimana, alisema taifa hilo limeweka mifumo dhabiti ya kukabiliana na msambao wa ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mawasiliano, utambuzi,  kuwafuatilia watu waliowasiliana na wagonjwa na matibabu ya ugonjwa huo.

Hadi kufikia sasa, watu zaidi ya 300 wameambukizwa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku takriban watu 60 wakifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo.

Waziri wa afya wa DRC Roger Kamba, amesema uwezo wa taifa hilo kukabiliana na Ebola umeimarika hasaa baada ya kupokea vifaa kutoka kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (CDC), pamoja na misaada mbali mbali ya kimataifa.

Share This Article