Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imemkamata na kumfikisha mahakamani mkurugenzi wa zamani wa maswala ya siasa katika serikali ya kaunti ya Taita Taveta kwa ufujaji wa fedha za umma.
Kwenye kesi dhidi yake, Geoffrey Kimonge Mbogo anadaiwa kujipatia shilingi milioni 8.3 kinyume cha sheria.
Mbogo, alikamatwa baada ya tume ya EACC kukamilisha uchunguzi na kisha kufikishwa kwenye mahakama ya kukabiliana na ufisadi mjini Voi.
Hata hivyo mshukiwa huyo alikanusha mashtaka hayo ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi dhidi yake.
Mahakama hiyo ilimwachilia Mbogo kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Kupitia ukurasa wa X, EACC ilisema kukamatwa kwa mshukiwa huyo ni ishara ya kujitolea kwake kulinda rasilimali za umma na kuwachukulia hatua wanaojihusisha na ufisadi pamoja na uhalifu wa kiuchumi.